Labda uko busy huwezi kupitia MAGAZETI ya leo TZ, ziko hizi stori 8 kwa ajili yako mtu wangu..
TANZANIA DAIMA
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufilisi (RITA), Phillip Saliboko amepandishwa Kizimbani Mahakama ya Kisutu akikabiliwa na shitaka la Rushwa ya Mil. 40 kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalila.
Wakili wa TAKUKURU, Dennis Lekayo amesema mshtakiwa huyo alipokea pesa hizo kama zawadi kutokana na kushughulikia suala la IPTL kwa Mamlaka aliyokuwa nayo wakati huo alikuwa kama mfilisi wa muda wa Kampuni hiyo.
Mkurugezi huyo alikana makosa hayo ambapo Wakili Lekayo amesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo akaomba apangiwe tarehe kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi April 9 mwaka huu na mshtakiwa huyo aliachiwa kwa dhamana.
TANZANIA DAIMA
Rais Kikwete amepokea Ripoti ya Ukaguzi ya CAG na kuagiza watumishi wote waliohusika kulipa mishahara hewa na kutumia vibaya pesa za Serikali wafikishwe Mahakamani, wafukuzwe kazi na washushwe vyeo ambapo Ripoti hiyo inaonesha kuna upotevu wa bil. 141 zilizolipwa kwa watumishi walioacha kazi, waliokufa na waliostaafu.
Katika taarifa ya CAG, Prof. Mussa Juma Assad amesema amebaini upungufu wa usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali ikiwemo kufanya malipo yasiyokuwa na nyaraka na kufanyika malipo yasiyoidhinishwa.
“Ukaguzi wangu pia umebaini kuwa mishahara ya watumishi walioacha kazi, waliofariki, waliostaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao”—Prof. Mussa Assad.
“Wanaotumia vibaya fedha za Serikali vibaya wachukuliwe hatua. Wenye ushahidi wa waziwazi wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya Sheria”—Rais Kikwete.
TANZANIA DAIMA
Mamlaka ya Mapato (TRA) imeongeza muda wa kubadilisha namba za usajili wa pikipiki na Bajaj hadi Desemba 31 mwaka huu kutokana na idadi ya vyombo hivyo kuwa kubwa ambapo taarifa ya TRA imehimiza wamiliki waharakishe kufanya usajili huo ili kuepuka usumbufu.
Utaratibu huu mpya ilikuwa ufanyike kwa miezi sita lakini Mamlaka hiyo imesogeza muda huo mbele zaidi, TRA imesema mfumo huu mpya ambao namba za vyombo hivyo utasaidia kupunguza wimbi la uhalifu.
Taarifa ya Mamlaka hiyo imesema utaratibu huu mpya vyombo hivyo vitakuwa na namba zinazoanza na ‘MC’ huku gharama ya kubadili namba hizo ni Tshs. 10,000/=.
TANZANIA DAIMA
Walimu wa Shule ya Msingi Mafizi iliyopo Kisarawe, Pwani wako hatarini kutokana na vyoo wanavyovitumia kudidimia ambapo kutokana na hali hiyo wamelazimika kujisaidia vichakani na wengine katika vyoo vya Zahanati.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Manyama Philipo amesema; “Kwa kweli sasa tuna changamoto ya vyoo.. mvua hizi zinazonyesha vyoo vyote vimetitia.. tuna hali mbaya”
Mmoja wa Walimu wa Shuleni hapo, Eveline Munisi amesema kutokana na jinsi hali ilivyo walimu wa kike wanalazimika kwenda porini wakiwa na majembe kwa ajili ya kujisaidia.
MTANZANIA
Siku chache baada ya Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Bagamoyo kuwakana Masheikh 50 waliokwenda Dodoma kumshawishi Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kugombea Urais, Masheikh hao wamejitokeza na kuthibitisha kwamba wao wanatambulika na BAKWATA.
“Tumesikitishwa na kauli ya Sheikh Mkuu kuwa haitambui safari yetu ya Dodoma wakati tulimtaarifu kabla na akatukubalia… ametugeuka baada ya vigogowa CCM kumfuata”, alisema Sheikh Kilemba, Msemaji Mkuu wa Masheikh hao.
“Hata Rais Kikwete hawezi kuniita Sheikh bandia mimi kwa sababu ananitambua nafasi yangu katika jamii… na nimemsaidia kama ninavyofanya leo kwa Lowassa”; alisema Sheikh Sharifu Muhidin Mapanga.
Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo hakuweza kupatikana kuzungumzia hili ambapo viongozi hao waliomtembelea Lowassa wameelekeza lawama kwake kwamba kawashushia hadhi Masheikh hao.
MTANZANIA
Serikali imetangaza kuvifunga baadhi ya vituo vya kulelea yatima kwenye Mikoa mbalimbali Tanzania kutokana na kukiuka Sheria uanzishwaji wake pamoja na vingine kubainika kuanzishwa ili kunufaisha wamiliki.
Mbali na hatua hiyo Serikali imesema inaendelea na uchunguzi ili kubaini vituo vingine ambavyo ni vya aina hiyo.
Kaimu Kamishna wa Haki za Mtoto, Steven Gumbo amesema kuwa uamuzi wa kuvifunga vituo hivyo umekuja baada ya kufanyika utafiti kwa Mikoa 25 na kubaini kuwa vituo hivyo viko zaidi ya 300 huku vingi vikiendeshwa bila leseni.
Akizungumzia kuhusu uamuzi huo, Ofisa wa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Hai, Helga Saimon amesema Wilaya hiyo ilikuwa na vituo zaidi ya 22 lakini ni vituo 7 tu ambavyo vilikuwa vikiendeshwa kwa kukidhi vigezo.
“Tulibaini mambo ya ajabu, kituo kimoja tulikuta mmiliki ni shoga na alikuwa akiwafanyisha watoto ushoga”—alisema Helga Saimon.
MWANANCHI
Profesa wa Chuo Kikuu Dodoma, Peter Kopoka amebanwa na uongozi wa chuo hicho kutokana na kushiriki maandamano ya kwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kumshawishi achukue fomu ya kugombea urais.
Profesa huyo akiwa na wahadhiri pamoja na watu wengine walioelezwa kuwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma walifanya maandamano hayo Machi 22, mwaka huu ambapo uongozi wa UDOM umemtaka ajieleze kwa nini ameshiriki harakati hizo za kisiasa huku akijua kuwa ni mtumishi wa umma.
“Ametuandikia barua ya kujieleza na kubainisha kuwa alikwenda yeye binafsi na siyo kama mwakilishi wa chuo… mambo haya ni magumu sana kutofautisha. Mimi kwa mfano, siwezi kwenda sehemu halafu nikasema sikwenda kama mkuu wa chuo… Lakini tumechukua maelezo yake na tumeyahifadhi,” alisema Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Kikula.
Kuhusu wanafunzi wanaodaiwa kushiriki harakati hizo kutoka chuoni hapo, alisema hakuna wanachoweza kufanya kwa sababu ni vigumu kuwatambua waliofanya hivyo na pia walifanya hivyo nje ya chuo, jambo linalowezekana.
“Maandamano hayo yalifanyika mtaani. Huko walikuwa wanavunja sheria za nchi, kama hawakufuata sheria, Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kudhibiti au kuruhusu jambo kama hilo kufanyika,” alisema Profesa Kikula.
Profesa Kopoka alikiri kuandika barua hiyo na kueleza kuwa alichokifanya ni kutekeleza haki yake ya uraia ya ushiriki katika utawala wa haki na demokrasia nchini.
“Nilikwenda kutokana na imani yangu kutokana na vile ninavyomfahamu Lowassa. Sikuwa peke yangu… walikuwapo pia wahadhiri kutoka vyuo vikuu vya Mtakatifu Yohana (St. John) na Mipango,” alisema Profesa Kopoka japo amesema pamoja na kufanya hivyo, suala hilo halijaathiri utendaji wake wala mkataba wake wa ajira.
Katika taarifa ya pamoja ya marais wa serikali za vyuo vikuu vilivyomo Dodoma imepinga kushiriki kwao na kubainisha kuwa waliofanya hivyo ni watu wa mtaani na sio wanafunzi kutoka Vyuo ambavyo vimetajwa.
MTANZANIA
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alizimia na kisha kukimbizwa hospitali wakati akihojiwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.
Gwajima ambaye alijisalimisha kituoni hapo saa 8 jana mchana akiitikia wito wa polisi uliomtaka kufika kutokana na tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Waandishi wa gazeti la Mtanzania Jumamosi waliokuwa kituoni hapo wanaeleza kuwa walimuona Gwajima akitolewa kutoka katika chumba cha mahojiano akiwa amebebwa na maofisa wa polisi alipelekwa moja kwa moja kwenye gari aina ya Noah kwa ajili ya kumpeleka hospitali.
Tukio hilo lililotokea majira ya saa 3 usiku ambapo muda mfupi uliopita Askofu huyo alionekana akiwa ameshikiliwa na wasaidizi wake kuelekea msalani huku yeye mwenyewe akiwa amejishika kichwa.
Msafara wake uliombeba ulikuwa ni wa magari mawili mojawapo ni Toyota Land Cruiser lenye namba PT 1848 na gari jingine ni Noah yenye namba T 215 BEM.
Akizungumza na gazeti hili kituoni hapo, mwanasheria wa Askofu huyo, John Mallya amesema wakati wakiwa katika mahojiano, alisema anahisi kizunguzungu na baadaye akaishiwa nguvu na akawa amefumba macho, polisi wakamchukua na kumpeleka katika hospitali ya Jeshi la Polisi iliyoko Kurasini ambapo baadaye Mwanasheria huyo alimtaarifu Mwandishi wa MTANZANIA kwamba walikuwa wakifanya mchakato wa kumuhamishia katika hospitali ya TMJ kutokana na hali yake kutokuwa nzuri.
Waandishi wa gazeti hilo walifika katika hospitali hiyo ya Jeshi la Polisi na kushuhudia Gwajima akitolewa katika hospitali hiyo na kupakizwa katika gari maalum la kubebea wagonjwa lenye namba DFP 6309.
Taarifa iliyolifikia gazeti hilo imesema Gwajima alikuwa hajala chochote hali ambayo iliibua wasiwasi kwamba huenda hiyo ilichangia kubadilika kwa afya yake.
Polisi mmoja aliyekuwa katika chumba cha mahojiano aliwaeleza waandishi kwamba Askofu Gwajima alipoteza fahamu muda mfupi baada ya kuhojiwa kuhusu mali anazozimiliki.
Gwajima alipofika kituoni hapo mchana kabla ya kuhojiwa alizungumza na waandishi wa habari ambapo alikiri kutoa lugha chafu dhidi Kardinali Pengo.
Wakati wa mchana Gwajima alifika polisi akiwa anatembea kwa miguu kutokana na foleni iliyokuwepo barabarani huku akiwa ameongozana na Mwanasheria wake John Mallya pamoja na baadhi ya wachungaji, waumini wa kanisa hilo na wengine waliotajwa kuwa ni walinzi wake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamishna Suleimani Kova alisema Mchungaji Gwajima ametii amri ya Jeshi hilo kama alivyotakiwa na baada ya kufika kituoni hapo alielekezwa kwenda kumuona Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP, Costantine Massawe.
Akitaja tuhuma zinazomkabili Mchungaji Gwajima, Kova alisema ni pamoja na kumkashifu na kumtukana hadharani kiongozi wa Kanisa Katoliki Kardinali Pengo.
No comments:
Post a Comment