STORI KUBWA ZAIDI KATIKA MAGAZETI YA LEO NI HIZIAPA, NI CHSCHE MUHIMU ZAIDI
MWANANCHI
Utata umeibuka kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada ya kiongozi huyo kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
Gwajima aliyetolewa kwenye chumba cha uangalizi maalumu cha Hospitali ya TMJ jana, amelitaka Jeshi la Polisi kurudisha bastola hiyo, akisema ni mali na aliiagiza ipelekwe hospitalini kwa sababu ya kujilinda.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo alipolazwa baada ya kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu akiwa katika mahojiano na polisi, Gwajima alisema anashangaa kukamatwa kwa wachungaji wake waliokuwapo kwa ajili ya kumlinda.
Hata hivyo, katika kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bunduki hiyo haina umiliki halali wa Gwajima wala wa wachungaji 15 waliokamatwa lakini baadaye jioni baada ya maelezo ya Gwajima, alitoa taarifa akisema bastola hiyo ni mali halali ya askofu huyo.
Pia alisema kuhusu risasi 17 za bunduki aina ya Shortgun, Gwajima anamiliki bunduki ya aina hiyo lakini akasema uchunguzi kuhusu watu hao 15 unaendelea.
Akizungumza kwa shida akiwa amejishika tumbo, Gwajima alisema alipopata taarifa za uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki dunia, aliagiza wachungaji waende hospitalini kwa ajili ya kumlinda, lakini wakaishia mikononi mwa polisi wakidaiwa kutaka kumtorosha.
Alisema alihofia kuwapo kwa watu wabaya ambao wangeweza kumdhuru halafu wakasingizia kitendo hicho kufanywa na polisi kwa kuwa alipata tatizo akiwa mikononi mwao.
“Usiku wasiwasi ulizidi, huku kila mmoja akiwa hafahamu kwa nini ujumbe wa namna ile unasambazwa kwenye mitandao, msambazaji ni nani, ana nia gani, nikaamua kuwaagiza waniletee silaha yangu iliyokuwa kwenye begi ili likitokea lolote niweze kujilinda,” Gwajima.
Alisema alishangaa kukamatwa wachungaji wake na kuchukua silaha iliyokuwa ndani ya begi na hadi jana hakuwa ameulizwa chochote kuhusu umiliki wa silaha hiyo.
“Kabla sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa kinachodaiwa kuwa nilitaka kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka kuzungumza na ZCO (Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi ya ile silaha ninayo,” alisema Gwajima.
Alisema madai kuwa alitaka kutoroka ilihali polisi alikwenda mwenyewe akitokea Arusha baada ya kusoma katika vyombo vya habari kuwa anatafutwa.
Alifafanua kuwa hata alipofika polisi kwa ajili ya mahojiano hakuwa na shaka hata kidogo, lakini alishangaa kuona anaishiwa nguvu kila baada ya muda na alipoona kichwa kinamuuma, akawaomba wampeleke hospitali ili mambo mengine yafuate baadaye, kitu ambacho hakikufanyika kwa wakati.
MWANANCHI
Vyombo vya usalama nchini Kenya, vinawashikilia wasichana watatu akiwamo Mtanzania, kwa kile kunachodaiwa kutaka kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Somalia.
Taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El -Wak, mpakani mwa Kenya na Somalia, Nelson Marwa amesema Mtanzania aliyekamatwa, alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan.
Mtanzania huyo, Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa kiongozi wa kundi hilo lililopanga kujiunga na al-Shabaab.
Wasichana wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.
“Hawa wasichana watatu, inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,” Kamishna Marwa.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athumani alisema: “Tunafuatilia hatujapokea taarifa zaidi ya hizo.”
Kamishna Marwa alisema raia hao wawili wa Kenya, mmoja ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya kilichopo Thika, Jimbo Kiambu na mwingine ni mwanafunzi wa Sekondari ya Burhania, iliyopo Malindi, Kilifi.
“Serikali imepata taarifa kuhusu watu wanaokusanya watu kutoka Afrika Mashariki ili wakajiunge na makundi ya ugaidi nchini Somalia, wakala wetu wa usalama wamepata taarifa hizo na kufanikisha kukamatwa kwa wasichana hao,” alisema Kamishana Marwa.
Hivi karibuni, tovuti ya al-Jazeera ilitoa taarifa za kukamatwa kwa mkanda wa video ulioonyesha mwakilishi wa kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Levant (ISIL) akimtaka kiongozi wa kundi la al-Shabaab kuliimarisha kwa kufanya mashambulizi ya kigaidi katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Kamishna Marwa alisema ingawa nyaraka za wasichana hao zote zinaonyesha kuwa ni wanafunzi, lakini bado walibanwa kwa maswali kuhusu sababu inayowapeleka nchini Somalia.
Aliongeza zaidi kuwa chanzo cha habari cha kiusalama kilieleza kuwa nyaraka za wasichana hao zilionyesha kuwa walikuwa wakienda kuolewa na wanajeshi wa kundi la al-Shabaab.
MWANANCHI
Wachambuzi wa soka wamesema timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ haina kiwango cha kuvutia uwanjani na imepoteza mvuto.
Wakizungumza baada ya kuishuhudia Taifa Stars ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Malawi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika Mwanza juzi, walisema wanauona mwisho mbaya wa kocha Mholanzi, Mart Nooij.
Kocha Joseph Kanakamfumu aliliambia gazeti hili kuwa Nooij hajaibadilisha Stars na inacheza ili mradi tu tofauti na mtangulizi wake, Kim Poulsen.
Kanakamfumu alisema jambo kubwa analokosea Mholanzi huyo ni uteuzi wa kikosi chake, hasa aina ya wachezaji anaowaita kwani wengi wao hawako fiti.
“Nikiangalia hajaibadilisha timu tofauti na wakati wa Kim kwani timu ilikuwa unaona kabisa inacheza mpira mzuri, lakini kwa huyu timu haichezi kwa mpangilio, hatuoni mtiririko mzuri uwanjani, kila mchezaji anajichezea anavyojua yeye,” alisema Kanakamfumu.
Aliongeza: “Tatizo kubwa anapokosea ni kwenye uteuzi wa timu yake, inatakiwa aangalie wachezaji anaowaita wapo vizuri namna gani kulingana na mfumo anaoutumia, kwani wachezaji wengi aliowaita hawaendani na mfumo wake wa kujilinda.”
Naye Eugine Mwasamaki alisema tatizo liko kwa kocha na hata wachezaji wake kwani kiwango cha timu hiyo si kizuri na kinasikitisha.
Mwasamaki alisema anachoshangaa ni Nooij kuwaita kikosini wachezaji ambao hata kwenye klabu zao hawachezi na kuwacha wengi wanaoonyesha viwango vizuri kwenye mechi Ligi Kuu Bara.
Wachezaji ambao hawana namba ya kudumu katika klabu zao kwa sasa, lakini wapo Stars ni pamoja na Mwadin Ally, Amri Kiemba, Deo Munishi na John Bocco.
MWANANCHI
Unakumbuka masaibu ya mtoto, hayati Nasra Mvungi aliyeishi kwenye boksi miaka mitatu? Mkazi wa Mbondole, Wilaya ya Ilala, Uwesu Mansuri (28) naye ameishi kwa kufungwa mnyororo mguuni na wazazi wake kwa miaka mitatu kwa madai ya kulinda usalama wake.
Kijana huyo ambaye anapata huduma zote za kibinadamu chini ya kibanda kidogo kilichopo chini ya mwembe nyumbani kwao, ameonekana kudhoofika na kutoa harufu mbaya kutokana na kutoogeshwa kwa muda mrefu.
Taarifa za kufungwa kwa kijana huyo zilisikika kutoka kwa wakazi wa eneo hilo na mwandishi wetu alifika eneo hilo na kushuhudia jinsi alivyofungwa na kuishi katika mazingira machafu.
Kijana huyo anakula na kujisaidia hapohapo, jambo ambalo limeelezwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuwa ni la unyanyasaji na hatari kwa afya yake.
Wakizungumza jana, wakazi wa eneo hilo walisema kijana huyo alifungwa mnyororo huo kwa zaidi ya miaka mitatu huku akiwa analala kwenye kibanda kidogo ambacho si salama kwake.
Mmoja wa wakazi hao, Imelda Saburi alisema wanaona uchungu kwa kitendo cha wazazi hao kumfunga mnyororo kijana huyo huku akipata maumivu makali yanayomfanya awe analia kwa sauti kila siku usiku.
Mmoja wa wakazi hao, Imelda Saburi alisema wanaona uchungu kwa kitendo cha wazazi hao kumfunga mnyororo kijana huyo huku akipata maumivu makali yanayomfanya awe analia kwa sauti kila siku usiku.
Alisema walijaribu kuwashauri wazazi hao wamfungue mnyororo huo na wampeleke hospitalini kupata huduma za afya lakini walikataa. “Tulimfuata baba wa mtoto huyo na kumshauri amfungue hiyo minyororo lakini alikataa ushauri wetu,” alisema Saburi.
Mkazi mwingine, Hassan Abdul alisema, wanashangazwa na wazazi hao kutojali huku wakimtenga na kumlaza nje akinyeshewa na mvua na kupigwa na jua.
Mama mzazi wa kijana huyo, Zuena Ngarima alisema walilazimika kumfunga mnyororo mguuni kwa kuwa amekuwa akifanya fujo na kuharibu vitu mbalimbali vya wakazi wa eneo hilo.
Alisema mwaka 2009, kijana huyo alianza kuchanganyikiwa na walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) na alilazwa kwa siku 19, alipopata nafuu aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Ngarima alisema wakati kijana huyo akipata ugonjwa huo, baba yake mzazi alikataa kumpeleka hospitalini akidai atapona, ndipo alipoamua kuwafuata ndugu zake na kumlazimisha amchukue ili akapatiwe matibabu. “Mwanangu amelazwa Muhimbili mara tatu lakini baba yake haonekani na huwa hachangii na kuniachia peke yangu nikimuuguza.”
Alisema kutokana na kukosa mtu wa kumsaidia kumhudumia kijana huyo, analazimika kutombadilisha nguo zilizochafuka kwa haja ndogo na kubwa jambo ambalo limemfanya awe anatoa harufu kali.
NIPASHE
Wafuasi 11 wa Chama cha Wananchi (CUF) wamevamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana wakati wakitokea katika mkutano wa hadhara wa chama hicho.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Fuoni Jitimai, wakati wakirudi nyumbani baada ya mkutano huo, uliofanyika Makunduchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Sadi, alisema watu wasiojulikana waliwajeruhi wafuasi hao, ambao walikuwa katika gari na majeruhi hao kukimbizwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na baadhi yao wamepewa ruhusa na wengine wamelazwa.
Kamanda Sadi alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kuwatia mbaroni waliohusika.
Wakati huo huo, Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salim, jana alilitaka Bunge lijadili kwa dharura hali ya amani visiwani Zanzibar kwa maelezo kuwa wanachama wa CUF, wamepigwa na kujeruhiwa.
Alisema kupigwa kwa wafuasi na wanachama wa CUF kunahatarisha amani visiwani humo na Tanzania kwa ujumla hivyo, akaliomba Bunge lijadili hali hiyo. Akijibu mwongozo huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimtaka aandike hoja yake na aiwasilishe kwa Katibu wa Bunge kwa njia ya maandishi.
NIPASHE
Mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, jana alitoa ushahidi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Khalid Kagenzi, za kutaka kumdhuru mumewe.
Kutokana na hatua hiyo ya Mushumbusi, Dk. Slaa alisema tayari wamefunga ushahidi kwa upande wake. Mushumbusi ambaye aliongozana na mumewe, Dk. Slaa walifika katika kituo hicho saa 4:00 asubuhi na kutoka saa 7:25 mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari baadaye, Dk. Slaa alisema alimsindikiza mkewe kituoni hapo kutoa maelezo akiwa shahidi yake.
“Leo mke wangu alikuja kutoa ushahidi. Na maelezo yote aliyoyatoa yameandikwa. Ameyapitia na mimi nimeyapitia. Hivyo, kwa upande wangu ushahidi nimekamilisha. Imebaki kwao tu kwa hatua zaidi pamoja na faili letu kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza: “Ninaomba ieleweke kwamba mke wangu ni shahidi na siyo mtuhumiwa kama ambavyo nimekwisha kueleza. Naomba msipotoshe kama ilivyotokea awali.”
Kwa upande wake, Mushumbuzi alisema wakati tukio linatokea, alishindwa kutoa ushahidi alipoitwa na Jeshi la Polisi kwa sababu alikuwa safarini, lakini baada ya kurudi alitoa taarifa kwa jeshi hilo.
“Wakati tukio linatokea, niliitwa kutoa ushahidi wangu, lakini sikufanya hivyo kwa sababu nilikuwa safari. Niliporudi niliwaambia, kwa hiyo wakaniambia nije leo,” Mushumbusi.
Aliongeza: “Maelezo ambayo nimeyatoa ni yale yale niliyosema kwenye vyombo vya habari. Kwa hiyo yameandikwa na nimeyapitia nikajiridhisha.”
Awali, akizungumza na waandishi wa habari juu ya wito wa mke wa Dk. Slaa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hakuwa na taarifa na jambo hilo na kwamba suala hilo linawezekana kwa kuwa ni utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi kwa jeshi hilo.
“Sina taarifa juu ya jambo hilo. Lakini hilo ni jambo la kawaida. Siyo jambo kubwa sana na ni utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi wa polisi. Na kama amekuja kuhojiwa ni wito, ambao anaweza kuitwa mtu mwingine yeyote,” Kova.
Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari, Mushumbusi alidai alibaini njama za Kagenzi ambaye alikuwa mlinzi wa Dk. Slaa, kutaka kumuua mumewe baada kukutwa na msaidizi wake wa ndani akiwa katika meza ya chakula, ambayo hutumika kwa ajili ya kuandalia chai ya mumewe japokuwa haikuwa kawaida yake kunywa chai katika meza hiyo.
Alisema hata hivyo, baada ya kukutwa na msaidizi wake wa kazi za ndani, Kagenzi alishtuka na kumwaga chai na hata alipoulizwa sababu za kufanya hivyo, hakutoa sababu za msingi.
Taarifa za awali za Kagenzi kutaka kumdhuru Dk. Slaa zilitolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, mbele ya waandishi wa habari, ambaye alieleza kuwa amekuwa akitumiwa na maofisa 22 wa vyombo vya usalama katika miaka miwili iliyopita kufanya mipango hiyo dhidi ya chama hicho.
Alidai Kagenzi amekuwa akitumiwa na maofisa usalama wa vyombo hivyo kupata taarifa nyingi za Chadema na kuziwasilisha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete ametunukiwa tuzo kubwa zaidi zinazotolewa na Umoja wa Vijana wa Afrika, kwa kutambua uongozi bora na mchango wake katika kuendeleza vijana.
Tuzo hiyo iitwayo “The African Youth Peace Award”, hutolewa na umoja huo kwa wakuu wa nchi na viongozi wa Afrika, ambao wamethibitika kuchangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa Waafrika.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilisema jana kuwa , Rais Kikwete alikabidhiwa tuzo hiyo na Rais wa Umoja huo, Francine Muyumba, wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Alikabidhiwa tuzo hiyo aliposimama kwa dakika chache kuwasalimia vijana wanaohudhuria mkutano wa tatu wa viongozi vijana wa Afrika na China, mkoani Arusha.
Muyumba alimweleza Rais Kikwete kama kiongozi mfano wa kuigwa kwa mchango wake katika kuwatambua na kuwaendeleza vijana katika nafasi za uongozi.
Rais Kikwete alikutana kwa mazungumzo na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, aliyekuwa jijini Arusha kufungua mkutano huo.
Alimshukuru Rais Mugabe kwa kukubali mwaliko wake wa kutembelea Tanzania ili kufungua mkutano huo.
Rais Kikwete pia alikutana kwa mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, Wang Jiariu, ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa vijana kutoka China kwa ajili ya mkutano huo.
HABARILEO
Wizara ya Nishati na Madini iko kwenye mchakato wa kukamilisha uandaaji wa sheria tatu, zitakazowasilishwa bungeni wakati wowote, zenye lengo la kuweka uwazi katika maeneo yote yanayohusu mikataba ya uchimbaji wa madini na gesi.
Aidha, wizara hiyo imetangaza kugunduliwa kwa gesi asilia ya futi za ujazo trilioni 1.0 hadi 1.8 katika kisima cha Mdalasini 1 mkoani Mtwara. Ugunduzi huo unaongeza kiwango cha gesi asilia iliyopatikana kwenye kitalu namba mbili na kufikia futi za ujazo trilioni 22.
Unafanya gesi asilia iliyopatikana nchini hadi sasa kufikia futi za ujazo trilioni 55.08. Akizungumza mjini hapa, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alitaja sheria zinazofanyiwa kazi kwa sasa ni ya uchimbaji, usambazaji na utafutaji. Sheria nyingine ni ya Uwazi na Uwajibikaji katika masuala ya madini na inayofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Petroli ya mwaka 1984.
Alisema sheria hizo zote zina lengo la kuhakikisha kila kitu kuhusu madini kuanzia uchimbaji, utafutaji wake na mikataba kinakuwa wazi, tofauti na ilivyo sasa ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Petroli mikataba yote ni ya siri.
“Najua watu wamekuwa wakipigia kelele uwazi wa mikataba, sasa hili tunataka tulifanyie marekebisho ya kisheria, kwa kuwa mimi kama waziri nimefungwa mikono siwezi kuweka hadharani kutokana na sheria kukataza hilo, nikiiweka wazi kampuni hizi zina uwezo wa kunishitaki na nitalipa mamilioni ya fedha,” Simbachawene.
Alisema ili kuendana na wakati na kasi ya ugunduzi wa gesi asilia nchini na nchi nyingine za jirani, ikiwa ni pamoja na ushindani wa soko la gesi, wizara hiyo inataka kuomba Bunge lifanyie kazi haraka sheria hizo, ikiwezekana kabla ya Bunge la bajeti.
“Wenzetu Msumbiji wamegundua gesi nyingi kuliko sisi, sasa tukiendelea kusuasua na jambo hili la sheria kwa mwaka mmoja pekee, tutaachwa sana nyuma, tunataka suala hili liishe muda si mrefu,” alisisitiza.
Hata hivyo, Simbachawene alisema si kweli kwamba mikataba iliyopo ilikuwa na usiri mkubwa, kama ilivyodhaniwa kwani mingi, ilikuwa ikiwasilishwa kwenye Kamati za Bunge na kupitiwa na wabunge.
Akizungumzia ugunduzi mpya wa gesi asilia, waziri huyo alisema kisima kilichogunduliwa gesi hiyo cha Mdalasini 1, kimechimbwa katika urefu wa meta za maji ya bahari 2,296 Kusini mwa Kitalu namba mbili chenye miamba yenye umri miaka 66 hadi 145.
HABARILEO
Utekelezwaji wa adhabu ya kifo kwa watu 10 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, kutokana na kuhusika katika mauaji ya watu wenye ulemavu (albino), unasubiri saini ya Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF).
Katika swali lake, Barwany, alitaka kufahamu ni lini utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa watu 10, waliokwisha hukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama kutokana na kuhusika na mauaji ya albino, itatekelezwa. Silima, alisema kwa mujibu wa taratibu za kisheria, adhabu ya kifo inapotolewa, utekelezaji wake husubiri saini ya Rais.
“Sijapata taarifa kama hukumu hizi tayari Rais ameziwekea saini ili zitekelezwe ila nitafuatilia ili Sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Katika swali la msingi la mbunge huyo, alitaka kufahamu hadi sasa kuna kesi ngapi za mauaji ya walemavu wa ngozi zilizokwishatolewa hukumu baada ya kufikishwa mahakamani na kesi ngapi bado zinasubiri huku na ni kwanini zimechelewa kutolewa maamuzi.
Waziri alisema kati ya mwaka 2006 na 2015, jumla ya matukio 56 ya uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa nchini na kati ya matukio hayo 41 yalihusisha vifo 43, matukio 13 yahusisha majeruhi na mawili ya kupotea watu hao albino.
Alisema kesi 46 kati ya matukio 56 zilifikishwa mahakamani na kesi 10 zenye watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu ya kifo na kesi 10 badi ziko chini ya upelelezi.
Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa huru kwa kukosa ushahidi. Silima alisema pia kesi 10 bado zinaendelea kusikilizwa mahakamani na ziko katika hatua mbalimbali.
“Kuhusu kuchelewa kwa hukumu au upelelezi wa baadhi ya kesi, kunachangiwa na sababu mbalimbali kama vile matokeo ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kutoka mamlaka za uchunguzi na mashahidi kutopatikana kwa urahisi na wakati”.
Katika swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum, Al Shamaar Kwegyir (CCM), alitaka kujua Serikali imefikia wapi katika kumtafuta mtoto Pendo Emmanuel mwenye ulemavu wa ngozi mkazi wa Kwimba, aliyechukuliwa mikononi mwa mama yake mzazi na mpaka sasa hajulikani alipo.
Akijibu swali hilo, Silima alikiri kuwa mpaka sasa Polisi inamtafuta na katika upelelezi unaoendelea jumla ya watu 14 wanashikiliwa na kuhojiwa kwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine na tukio hilo, akiwemo.
No comments:
Post a Comment