Kutoka kwenye MAGAZETI ya leo March 30, hapa kuna stori 9 zilizopewa headlines
MWANANCHI
Leo Serikali itawasilisha muswada bungeniwa sheria ya makosa ya mitandao wa mwaka 2015 kwa hati ya dharura unaoorodhesha adhabu mbalimbali ikiwemo ya faini ya milioni 50 au kwenda jela miaka saba kwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono mitandaoni.
Baadhi ya makosa yaliyoanishwa katika sheria hiyo ni kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono bila ridhaa ya mtu,kusambaza picha za ngono na za utupu,udanganyifu unaohusiana na kompyuta na kusambaa picha za utupu za watoto.
Mengineni unyanyasaji kupitia mitandao,kusambaza picha yoyote ambayo itasababisha mauaji ya kimbari,uongo na matusi ya kibaguzi.
Sheria hiyo katika kifungu cha 48 inaipa mahakama mamlaka ya kutaifisha mali iliyopatikana kutokana na kosa lililofanywa na mhusika,sheria hiyo pia itawataka wote watakaobainika kufanya makosa hayo kuwasilisha hati zao za kusafiria kwa mamlaka husika hadi hapo watakapolipa faini au watakapokuwa wamemaliza kutumikia kifungo.
NIPASHE
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Positive Thinkers Tanzania (PTT), umeonyesha kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anaongoza kati ya wanaotajwa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Utafiti huo pia unamuweka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa katika nafasi ya pili.
Matokeo ya utafiti huo yamewapa nafasi za juu wanasiasa hao baada ya utafiti wa Shirika lisilo lwa kiserikali la Twaweza mwaka jana kumpa Lowassa nafasi ya kwanza na Dk. Slaa nafasi ya tatu.
Utafiti wa PTT yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, matokeo yake yaliyotangazwa jana yanaonyesha kuwa Lowassa alipata kura 752 kati ya 3,298 zilizopigwa.
Dk. Slaa alipata kura 644 na Naibu wa Fedha, Mwigulu Nchemba 350.
Akitangaza ripoti ya utafiti huo jijini Dar es Salaam, Rais wa Taasisi hiyo, Tibatizibwa Gulayi, alisema ulifanywa katika mikoa 13 kwa kuwauliza wananchi kwa njia ya madodoso kisha taarifa zake kuingizwa katika mfumo wa Elektroniki unaojulikana kama Fast web application system (FWAS).
Alisema kuwa utafiti huo ulianza Februari, mwaka huu na kumalizika mwanzoni mwa Machi, mwaka huu na ulihusisha majina wanasiasa 15 wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.
Gulayi alisema wanasiasa wengine waliotajwa na kura zao kwenye mabano ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba (294); Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (227); Kiongozi Mkuu wa ACT – Tanzania, Zitto Kabwe (224); Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (197); Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (107) na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (72).
Wengine ni Naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (54); Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya (40); Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia (34) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi (31).
Waliofuatia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (16) na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye (10).
Watu ambao walisema hawana mgombea walikuwa 79 wakati waliosema mgombea yeyote atakayegombea ni sawa walikuwa 167.
Katika utafiti huo makundi mbalimbali ya watu wenye umri kuanzia miaka 18 walihojiwa. Makundi hayo yanahusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu, wanazuoni na wananchi wa kawaida.
Gulayi alitaja mikoa iliyohusika kwenye utafiti huo kuwa ni Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Tanga, Lindi, Dodoma, Pwani, Iringa, Kilimanjaro, Shinyanga na Morogoro.
“Watu waliokwenda katika mikoa hiyo walitakiwa kuwahoji wananchi nani anaweza kutuongoza kwa kuangalia uwezo wa muhusika katika utendaji wake kwa vitendo, kupambana na ufisadi na Rushwa,” Gulayi.
Hata hivyo, alisema utafiti huo ambao haukuegemea upande wowote wa kisiasa, ulifanywa kutokana na hamasa za wananchi kutaka kujua hali ya mtazamo, vigezo na matarajio ya watu katika kumchagua kiongozi wao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Alisisitiza kwamba utafiti huo umevunja dhana ya wananchi na wanasiasa wengi wanaodhani kuwa viongozi wa kisiasa wanategemea idadi ya wanachama na watu wenye mlengo wa itikadi unaofanana.
Lakini alisema kuwa watu walipiga kura katika utafiti huo bila kujali mtu ana itikadi ya chama gani.
“Wananchi wameanza kupata mwanga na weledi katika kufanya maamuzi chanya katika kuwachagua viongozi wanaowahitaji,” alisema Gulayi.
NIPASHE
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, wameweka hadharani mali, maslahi na madeni, ambazo zitawekwa wazi kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na tovuti ya chama ili wananchi wasome.
Akihutubia mamia ya wananchi wakati wa uzinduzi wa chama hicho, Zitto alianza kwa kuweka hadharani mali zake mbele ya mwanasheria wa chama na kudai kwa undani zitawekwa kwenye mtandao ili kila mwananchi ajisomee.
Kabla ya kusaini fomu hiyo, Zitto alisema Watanzania wananyanyapaliwa na kupuuzwa huku uchumi kushikiliwa na wachache na kwamba kwa sasa ni muda wa uchumi shirikishi kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao.
Alisema wananchi waikatae Katiba inayopendekezwa kwa kuwa imeshindwa kuwa na mfumo wa kuwajibisha na uwajibikaji kwa viongozi wa umma.
Alisema Tanzania inapoteza kiasi cha Sh. bilioni 490 kutokana na ushuru wa forodha huku kiasi cha Sh. trilioni mbili kila mwaka kikipotea kutokana na misamaha ya kodi, fedha ambazo zingetatua matatizo ya watanzania.
Awali, Mwenyekiti wa chama hicho, Anastazia Mghwira, alisema nia ya chama hicho ni kuhakikisha Taifa kwanza, sasa, leo na kesho ili kurejesha heshima ya Mtanzania ya undugu na kujali.
Mghwira alisema ni mara ya kwanza kwa chama cha siasa kuongozwa na mwanamke na kwamba chini ya uongozi wake watahakikisha tafsiri za rasilimali za Taifa inaonekana katika maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Samson Mwigamba, alisema kwa kipindi cha miezi saba chama hicho kimejiimarisha na kupata wenyeviti 13 wa mitaa, vijiji 13, vitongoji 67 na wajumbe wa serikali za mitaa na vijiji 250, hivyo kushika nafasi ya tano kati ya vyama 22 vya siasa.
Mhasisi wa chama hicho, Prof. Kitila Mkumbo, alisema moja ya matatizo ya vyama vingi vya siasa ni kuchanganya uongozi wa chama na dola, na kwamba vyama vyenye akili kama ACT kinakuwa na kiongozi wa chama na viongozi wengine.
Alisema ndani ya chama hicho cheo siyo jambo la msingi sana bali muhimu ni majukumu na kwamba moja ya kazi kubwa ya kiongozi mkuu ni kutangaza ilani ya chama na kuwasilisha taarifa kwa Mwenyekiti.
NIPASHE
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye , amefunguka kuhusu uamuzi wa Umoja wa Vijana wa CCM makao makuu kusitisha shughuli za kumsimika kuwa Kamanda wa Vijana wa Wilaya ya Hanang.
Akizungumza na maelfu ya wakazi wa mji wa Katesh juzi, alisema ni mawazo potofu kufikiri kwamba anahitaji ukamanda ili azunguke popote na hasa katika wilaya hiyo.
Mkutano huo ulitanguliwa na maandamano ya wananchi huku wengine wakiwa kwenye pikipiki na magari na pamoja na vikundi vya ngoma huku wengine wakiwa wamejipanga barabarani.
Maandamano hayo yalianzia nyumbani kwake Endasak hadi viwanja vya mkutano vilivyopo jirani na kituo cha mabasi.
Alisema jambo hilo halimshangazi kwa sababu alishapewa habari kuwa baadhi ya vijana hao walioandaliwa walikuwa wakisema hataapishwa mpaka baada ya uchaguzi mkuu upite.
“Nikajiuliza uhusiano ni nini kati ya ukamanda na uchaguzi mkuu.
“Nimedokezwa na hii ingekuwa hisia ya mtu ye yote kuwa ati mimi nitatumia nafasi hiyo ya ukamanda kuzunguka wilayani kupinga mtu fulani au watu fulani wasichaguliwe,” alisema bila kumtaja.
Alisema msimamo wake ni kutogombea ubunge wa jimbo hilo, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Dk. Mary Nagu (CCM).
Alisema anao vijana wengi tena wasomi katika jimbo hilo ambao anawaachia wagombee nafasi ya ubunge badala ya yeye katika umri mkubwa wa miaka 60 aliyonayo kung’ang’ania kugombea.
“Nimekuwa mbunge wa jimbo hili kwa miaka 20 mfululizo, sasa hivi kuna vijana wengi tena wasomi wanaweza kugombea. Siwezi kugombea ubunge, ninyi mnajua mimi nataka kugombea nini, au kuna mmoja hajui hilo?”
Alisema yeye mpaka sasa anashikilia rekodi ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza aliyekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo na ametoka madarakani akiwa hana kashfa.
“Mnajua misingi ambayo nimekuwa ninasimamia na ninaendelea kuisimamia hadi leo…nimekuwa napigania maendeleo, umoja, upendo na amani.
“Ni mpambanaji dhidi ya dhuluma, kugawa jamii kwa misingi ya ukabila au siasa na sina simile na rushwa, ufisadi na maovu mengine katika jamii,” alisema.
Alisema alishangaa kupata taarifa kuwa UVCCM makao makuu Dar es Salaam wametoa taarifa ya kusitisha shughuli ya kumwapisha kwa maelezo kuwa kuna malalamiko hadi hapo baadaye wakati ilishatangazwa na UVCCM wilaya ya Hanang’.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alipoulizwa jana kuhusiana na kusitisha kumwapisha Sumaye, alisema alikuwa katika mkutano wa vijana jijini Arusha na kuahidi kuzungumza baadaye.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia wafuasi 15 wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa tuhuma za kutaka kumtorosha Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Josephat Gwajima.
Gwajima ambaye amelazwa katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni Dar es Salaam, baada ya kupata mshituko wakati akihojiwa na makachero wa Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, ilisema usiku wa kumkia jana, mmoja wa walinzi wa Hospitali ya TMJ alibaini njama za kutaka kutoroshwa kwa Askofu Gwajima ambapo alitoa taarifa polisi.
“Kutokana na hali hii, makachero wa polisi walifika eneo hilo na kukuta kweli kuna hali ambayo si ya kawaida kwa kuwapo kundi la watu.
“Wamekamatwa watu 15 na mmoja wao Ekomia Diagare, alikutwa na begi ambalo lilikuwa na vitu mbalimbali ambayo alidai anampelekea Askofu Gwajima.
“Bastola aina ya Bereta yenye namba CAT 5802 ikiwa na risasi 3, risasi 17 za Shortgun, vitabu, hundi za benki, hati ya kusafiria yenye jina Gwajima Mathias Joseph yenye namba AB54480,”Kamanda Kova.
Mbali na hilo, pia inadaiwa watu hao walikutwa na kitabu cha Benki ya Equity na hundi, nyaraka mbalimbali za Kampuni ya Puma, chaja za simu na suruali mbili, makoti mawili, fulana za ndani moja,soksi jozi mbili na nguo ya ndani.
Wakili wa Askofu Gwajima, John Mallya kuhusu taarifa hizo, alikiri kukamatwa kwa watu hao kutokana na njama hizo.
MTANZANIA
Serikali imetenga Sh trilioni 14 kwa ajili ya kujenga reli mpya yenye urefu wa kilometa 2,561 ambayo itakuwa na kiwango cha kisasa cha ‘Standard Gauge’, ambao utakuwa mradi mkubwa kutekelezwa na Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, alisema reli hiyo mpya itakuwa tofauti na nyingine na yenye uwezo wa kimataifa kutokana na kuchukua mabehewa ya ghorofa, ambapo itaanzia Dar es Salaam hadi Kigoma.
Treni hiyo itapita katika mikoa ya Tabora, Mwanza, Isaka hadi Rusumo, Kaliua-Mpanda – Karema na Uvinza hadi Musongati nchini Burundi.
Sitta, alisema pamoja na masuala mengine, reli hiyo itasaidia kukidhi mahitaji makubwa ya ubebaji mizigo kwenda nchi jirani za DRC, Rwanda, Burundi na Uganda lakini pia itasaidia usafirishaji wa wananchi wetu kwenda mikoani kwa wingi na kasi zaidi.
Alisema serikali imeamua kujenga reli mpya kwa kuwa iliyopo ni ya kiwango cha ‘Meter Gauge’ ambapo uwezo wake ni mdogo kwani kwa mwaka ni tani milioni tano, ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo katika kanda hiyo ambayo yatafikia tani milioni 30 ifikapo 2025.
“Tunahitaji kukabiliana na uongezekaji wa mizigo kwa kujenga uwezo wa kuihudumia kwa kuwa na reli ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba mizigo hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe lakini pia kwa kasi ya wastani wa kilometa 100 hadi 120 kwa saa hivyo kuwezesha abiria kufika haraka zaidi sehemu wanazokwenda,” alisema.
Alisema reli hiyo itapeleka mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam mpaka nchini DRC Congo ambapo itachukua muda wa saa 12.
Alisema uzinduzi wa reli hiyo utafanywa Juni 30, mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete kwa kuweka jiwe la msingi eneo la Mpiji kituo cha stesheni Mkoa wa Pwani ambako ndipo utaanzia ujenzi.
Alisema uzinduzi wa reli hiyo utafanywa Juni 30, mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete kwa kuweka jiwe la msingi eneo la Mpiji kituo cha stesheni Mkoa wa Pwani ambako ndipo utaanzia ujenzi.
Alisema kwa ujumla reli zote tatu zitagharimu shilingi trilioni 26 na zitaajiri watanzania milioni moja kwa miaka yote zitakapokuwa zinajengwa kutoka 2015 hadi 2021.
Akizungumzia hatima ya Kaimu Mkurugenzi aliyesimamishwa kwa muda wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande, Sitta alisema uamuzi wa ripoti ya uchunguzi utatolewa wiki hii.
MTANZANIA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, amesitisha kuanza kwa mradi wa mji mpya Kigamboni hadi pale mikataba itakapopitiwa upya.
Pamoja na hali hiyo Lukuvi, amewataka wananchi wa maeneo hayo kutouza ardhi yao kwa sasa.
Ahadi ya hiyo aliitoa jana katika mkutano na wananchi wa Kigamboni baada ya kutokea kutoelewa baina ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka na wananchi kuhusu ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.
Kutokana na hali hiyo Waziri Lukuvi aliwataka wananchi hao kutouza ardhi yao kwa wakati huu na kusubiri wakati muafaka baada ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kukamilika na kutangazwa kimataifa hivyo kuifanya ardhi hiyo kuwa na hadhi.
Alisema kuna watu katika kipindi hiki wanapita na kuwataka wananchi wa Kigamboni kuuza ardhi yao na kuwadanganya kuwa Serikali itachukua maeneo yao kwa bei ya chini.
“Serikali haina mpango wa kuchukua ardhi kwa bei yoyote bali inahitaji kuona maendeleo, na kila wakati ukifikia kila mmoja atauza ardhi yake kwa thamani ya Mji mpya sio sasa wanavyowadanganya, hao ni matapeli.
“Najua ipo siasa nyingi ya itikadi za CCM na CUF lakini zote hazitasaidia zaidi ya kusubiri ‘Master Plan’ ambayo yenyewe ipo na sera za kiuchumi zaidi, hivyo kila mmoja ahakikishe anakuwa na hati ya eneo lake,” Lukuvi
Hata hivyo baada ya wananchi wa waliohudhuria mkutano huo kuonyesha hofu juu ya kauli Lukuvi, ambaye aliwatoa shaka hiyo na kuwaahidi kurekebisha chochote kinacholeta kutoelewa kati yao na Serikali.
“Mpango niliowaambia mimi ndio unaotakiwa kuwa lakini kama kuna jambo lipo tofauti na nyaraka ambazo mnazo nyinyi sio tatizo tutashughulikia, inawezekana kuna mambo hayakutekelezwa ipasavyo.
“Tutapitia nyaraka zote tuone kama ni za kisheria au ziliandikwa tu na waziri, kama ni waraka tu wa waziri nitarekebisha kwani na mimi ni waziri nina uwezo wa kuondoa yasiyo mazuri lakini kama ni la kisheria bado tuna mabunge mawili tutalipeleka bungeni ili lirekebishwe,” alisema
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar esa Salaam , Saidi Mecky Sadiki, aliahidi kushirikaiana na wizara katika suala la wananchi wa Kigamboni na kuitaka wizara hiyo kuanzisha dawati maalumu litakaloshughulikia kutoa hati kwa wakazi wa maeneo hayo ya Kigamboni.
MTANZANIA
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana nusura wazichape kavukavu baada ya kutofautiana juu ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.
Hali hiyo ilijitokeza wakati wabunge hao wakiwa katika semina iliyohusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, ambapo miongoni mwa sheria zilizomo ndani yake ni pamoja na ile ya Mahakama ya Kadhi.
Sakati hilo lilitokea katika semina kuhusu muswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni keshokutwa iliyofanyika katika Ukumbi wa Msekwa, mjini hapa.
Licha ya badhi ya wabunge kutaka kunyanyuka kwenye viti vyao na kwenda kupigana, wapo waliokuwa wakirushiana maneno makali.
Semina hiyo ilianza katika hali ya utulivu, lakini baada ya muda hali ya hewa ilichafuka baada ya baadhi ya wabunge kusimama na kupinga sheria hiyo.
Hali ilibadilika baada ya Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), aliposimama na kuchangia ambapo aliunga mkono muswada huo.
Katika mchango wake, Jafo aliwashangaa Wakristo kujifanya wazungumzaji wakubwa kuhusu suala hilo la Mahakama ya Kadhi wakati jambo hilo haliwahusu.
“Nataka niwaambie Serikali msije mkafanya masihara Muswada huu usiingie bungeni, muswada uje tutafanya ‘Amendment’ (marekebisho) huko na naitahadharisha Serikali iwe makini katika hili,”Jafo.
Alipokuwa akichangia, baadhi ya wabunge walikuwa wakimzomea na kusababisha mbunge huyo kususa kuendelea kuchangia ambapo alilazimika kwa kuwataka wabunge waislamu wakutane nje baada ya kumalizika kwa semina hiyo.
Kauli ya Jafo ya kuwataka wabunge Waislamu kukutana baada ya semina ilionekana kuwachefua baadhi ya wabunge ambapo walisimama na kupinga kauli hiyo, huku wengine wakitoka nje ya ukumbi huo.
Wabunge waliosimama na kuanza kumpinga Jafo ni pamoja na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) na Mbunge wa Nyamagana, Hezekiah Wenje (Chadema)
Wakati hali hiyo ikiendelea, Mbunge wa Chwaka, Yahaya Kassim Issa (CCM) na Mbunge wa Konde, Khatibu Saidi Haji, (CUF) walisimama na kutaka kwenda kumshambulia Machali, kabla ya kuzuiwa na wenzao waliokuwa wamekaa nao jirani.
Hali hiyo ya vurugu na makelele iliendelea kwa takribani dakika 10, huku baadhi ya wabunge wakitaka semina ivunjike.
Wakati vurugu hizo zikimshinda aliyekuwa Mwenyekiti wa semina hiyo, William Ngeleja, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo, walikua wameketi kwenye viti vyao huku Spika Anne Makinda akilazimika kusimama na kuanza kuwatuliza wabunge hao.
Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alisema katika katiba Ibara ya 19 ilishaweka wazi kuhusu suala la uhuru wa kuabudu kwamba jumuiya zote za kidini zitakuwa nje ya mamlaka za nchi.
Mwenyekiti wa kikao hicho (Ngeleja) alimtaka Ndasa avute subira kusikia maudhui ya semina hiyo huku akisisitiza kwamba hakuna kipengele chochote cha Katiba kilichovunjwa.
Mbunge wa Ngara, Deogratius Ntukamazina (CCM), alisema yeye kama mjumbe wa Kamati ya Bunge Katiba na Sheria walikutana na makundi 11 ya masheikh lakini yaliukataa muswada huo.
“Waislamu hawa walisema wao hawaitambui Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania), naiomba Serikali kwa jambo hili kubwa la Mahakama ya Kadhi hamuwezi kulileta kwa marekebisho madogo kama haya.
Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF), alipinga kitendo cha mahakama hiyo kuanzishwa chini ya uratibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kwa madai kwamba ni taasisi ya mtu binafsi iliyosajiliwa na Rita kama zilizovyo taasisi nyingine.
“Suala hili halikubaliki, kwa nini Mahakama ya Kadhi iundwe chini ya Mufti, au Waziri Mkuu anataka tu kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi kwa kuwa alishaahidi, msitake kuipasua hii nchi.
“Kama waziri mkuu yeye aliahidi kwa ajili ya kuutafuta urais shauri yake ila ni marufuku kuwalazimisha watu kuwa chini ya Bakwata, kufanya hivyo ni kukiuka Katiba.
MAJIRA
Jeshi la Magereza nchini, limemfukuza kazi askari wake wa Gereza la Bariadi, mkoani Shinyanga kwa kosa la kupatikana na fedha za bandia kinyume cha sheria.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkaguzi wa Magereza, Lucas Mboje na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Minja, ilimtaja askari huyo kuwa ni Namba B. 6499 Wdr. Edmund Masaga.
Alisema askari huyo amefukuzwa kazi kwa fedheha kuanzia Machi 28 mwaka huu kwa kosa la kulidhalilisha jeshi hilo kinyume na Kanuni za Utumishi wa Jeshi la Magereza za mwaka 1997.
Katika taarifa hiyo, Kamishna Jenerali Minja alikemea vitendo hivyo ambavyo alisema ni kinyume cha maadili na utendaji ndani ya Jeshi la Magereza.
Hata hivyo aliwataka askari wote nchini kutenda kazi zao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.
Wiki iliyopita polisi mkoani Simiyu liliwakamata askari wawili wa jeshi la magereza baada kukutwa na noti bandia ikiwa ni pamoja na sare za jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ).
Akitoa taarifa za kukamatwa kwa askari hao, Kamanda wa polisi mkoani humo, Naibu Kamishina, Charles Mkumbo alisema askari hao walikamatwa saa 9 mchana katika Mtaa wa Old Maswa Kata ya Nyakabindi wilayani Bariadi.
Baada ya askari hao kukamatwa mmoja wao, PC Juma alipopekuliwa katika mfuko wa suruali yake alikutwa na noti nyingine za bandia za elfu kumi na jumla yake kama zingelikuwa halali zingelikuwa na thamani ya Sh 1,920,000.
No comments:
Post a Comment