KASHFA NZITO HOSPITALI YA SINZA PALESTINA WAMUUA MTOTO KWA UZEMBE, MGANGA MKUU ACHANGANYIKIWA ASEMA YUPO TAYARI KUWAJIBISHWA KWA TUKIO HILI.
Na Livingstone Mkoi Mwandishi Habari za Uchunguzi wa
E-FM Radio
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na kushtua hospitali ya Sinza-Palestina imekumbwa na kashfa nzito ya kusababisha kifo cha mtoto mchanga baada ya kutokana na uzembe wa hali ya juu.
Habari zaidi toka kwa mama mzazi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Elizabeth Kimaro, mwenye miaka 40, zinadai kuwa, tarehe 22 mwezi huu (Machi) alishikwa na uchungu majira ya saa tisa usiku na asubuhi kulipokucha mdogo wake aliyefahamika kwa jina la Msiyaka alimpeleka hospitali hiyo ya Palestina kwa ajili ya huduma zaidi.”
Akisimulia kwa majonzi makubwa, mama huyo ambaye ni mkazi wa Mabibo aliendelea kusema kuwa, akiwa hospitalini hapo, baada ya kupokelewa na madaktari, alipimwa na kumwambia kuwa, hana tatizo lolote na kwamba alielekea kujifungua bila shida huku wakimsisitizia kuwa njia inafunguka vizuri japo alikuwa amekaa muda mrefu bila kuzaa.
Akaendelea kusimulia kuwa, baada ya kumaliza kumpima, mama huyo anadai akaendelea na mazoezi mepesi kusubiri mtoto ashuke na ilipofika muda wa saa tatu usiku, kuna wahudumu waliokuwa wamempokea tangu asubuhi muda wao ulikuwa umekwisha, wakaondoka na yeye alikabidhiwa kwa dada mwingine mhudumu wa zamu ya usiku.
Hata hivyo, mama huyo anasema wahudumu wa zamu ya mchana walikuwa na moyo wa kibinadamu na huruma ya hali ya juu kwani aliwaona wakipigania kuokoa maisha ya akina mama na watoto wao huku akiwataja majina ya Elizabeth na Hyasinta.
Mama huyo anasema wahudumu walioachwa zamu ya usiku ni watoto wadogo wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 na 20 na ndio walionekana mara moja kuzungukazunguka kwenye wadi ya wajawazito (leba) kuwahudumia waonasubiri kujifungua huku leba hiyo ikiwa haina umeme kabisa.
Aidha, mama huyo aliendelea kueleza kwa uchungu kuwa, wakati hayo yanaendelea, wahudumu watu wazima walikuwa wamekaa upande wa pili wakinywa kahawa na kutafuna kashata licha ya yeye kuwaita mara kwa mara, lakini, aliishia kujibiwa; “Wewe unapiga kelele tangu umefika hapa, unaitaita tuuu, kwani mtoto ameshatoka tayari?”
Mama huyo alizidi kusema kuwa, baada ya kuona amezidi kupiga kelele za kuomba msaada kutokana na mtoto kuanza kushuka, mkuu wa wahudumu hao alimtuma mhudumu mmoja binti aende kumtazama na baada ya nesi huyo kufika alimwambia kuwa kama taa hakuna basi achukuke simu yake ya mkononi atumie tochi imsaidie kumtolea mkojo uliokuwa umembana sana.
Hata hivyo, nesi huyo kijana alipochukua simu hiyo ili akachukue mpira na kurudi kwa kutoa mkojo, kabla hajamtoa mkojo, tayari mtoto alikuwa njiani kutoka na ilibaki kusukuma tu na mtoto alikuwa mzima, lakini, alikuwa amechoka kutokana na kukaa muda mrefu kwani mtoto ilikuwa azaliwe saa tatu lakini amezaliwa saa tano na dakika kadhaa.
Mama huyo anaendelea kusema, alikuwa kila akiwaeleza manesi wamsaidie, walimwambia ajigeuze tu, hata ubavu, kwa vile mtoto alikuwa anatoka, huku wao wakimalizia kwa vicheko vya kejeli.
Kadhalika, mara ya pili yule nesi aliporudi alichukua tochi ya simu yenye mwanga kwani wao hawakuwa na simu zenye mwanga mkubwa (smart phone) na baada kufika kwa huyo mama, tayari mtoto alikuwa kishazaliwa.
Elizabeth hapa anasema, kwa kweli hili hata akiitwa kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk.Seif Rashid atasema hata kwa kuapishwa kwa kitabu cha imani yake baada ya yule mhudumu kufika pale na kukuta mtoto amezaliwa huku akiwa amechoka, alimuokota mtoto na kumuingiza mipira puani kwa nguvu, basi hapo damu nyingi kama bomba zilianza kumtoka mtoto puani na yule mhudumu alivyoona hali ile alishtuka na kusema; ‘Mungu wangu’.
Baada ya hapo mhudumu huyo alichukua khanga na kumwambia eti ngoja ampeleke sehemu ya mwanga huku damu zikiendelea kulowesha khanga na baada ya kumpeleka mtoto huyo mhudumu huyo alirudi tena na ile simu yake akiendelea kusaidia akina mama wengine na hakuhangaika naye tena licha ya kuhitaji msaada wa kukamuliwa damu tumboni ili kutoa uchafu.
“Yaani sikupata msaada wowote, yule binti nesi aliendelea kuhangaika mwenyewe usiku mzima kwa kuwazalisha akina mama wajawazito wengine,” analalamika Elizabeth.
Hata hivyo, mama huyo anasema kumbe kipindi mwanae alikuwa ameshapoteza maisha wala wasimwambie, lakini, cha kushangaza ni baadae aliwaona wahudumu kama watano wakiwa ‘bize’ na wagonjwa akajiuliza kumbe wahudumu wote wapo iweje akina mama wapate shida kiasi kile hata kusababisha watoto kupoteza maisha?
Mama huyo anasema, licha ya uzembe wa wahudumu kusababisha kifo cha mtoto wake, lakini, pia lawama nyingine anazipeleka moja kwa moja kwa uongozi wa hospitali kwa kushindwa kuweka umeme hata wa dharura katika ‘leba’ ikizingatiwa ni mahala muhimu kuwa na umeme wakati wote.
Aidha, mama huyo anadai kuwa, alipomaliza wahudumu hao walimjibu: “Hili ni tatizo la muda mrefu, hii ndio serikali yenu, kwanza hospitali hizi hazina vifaa, someni ubaoni walivyoandika wenyewe kwa uzembe wao, hairuhusiwi kwa mama yeyote mjamzito kutoa rushwa, eti, vitu vyote ni bure! Uchungu nao ni shilingi ngapi? Eti tusaidiane!!!”
Mama huyo anasema baada ya mwanae kupotea mhudumu huyo alikuja kumuweka wazi kuhusu kifo cha mtoto na alipomuhoji sababu ya mwanae kufariki, mhudumu aliongopa kuwa eti mtoto wake alizaliwa akiwa amejisokota shingoni jambo ambalo hakubaliani nalo kwa kuwa kwake haikuwa mara ya kwanza kuzaa na hata walipokabidhiwa mwili wa mtoto huyo haukuwa na alama ya kamba kujisokota zaidi ya damu nyingi puani.
Kufuatia tukio hilo, licha ya mama huyo ambaye ni mfuasi wa ulokole kutaka kusamehe suala hilo, familia yake imemkatalia mama huyo na kusema watafika nalo mbali ili kukomesha ukatili unaoendelea kwenye hospitali hiyo. Aidha, kutokana na mama huyo kuwa katika hali ambayo haijatengemaa kutokana na kifo cha mwanae, alipandwa na presha na hadi sasa bado hali yake ni mbaya.
Nacho kituo cha E-FM Radio 93.7 kupitia kwa Kitengo Maalum cha Habari za Uchunguzi, hatua ya awali kimepiga hodi kwa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dokta Luoga ambaye ameshtushwa na tukio hilo kwa vile alikuwa amepewa ripoti tofauti juu ya kifo cha mtoto huyo na wasaidizi wake.
“Jamani, haya mbona makubwa, taarifa za kifo cha mtoto huyo hizi mezani kwangu, lakini, ziko tofauti na haya maelezo ya huyo mama,” alisema Dokta Luoga ambaye kipindi hicho alikuwa akisikilizishwa sauti ya mama huyo iliyorekodiwa.
Aidha, mganga huyo baada ya kuandika maelezo hayo, aliitisha kikao cha dharura na wakuu wa hospitali hiyo wakiwemo wale wa Ustawi wa Jamii na kusikiliza tuhuma hizo na kuchukua maelezo ambapo maganga huyo alisema kuwa, apewe muda wa siku mbili tatu afanye uchunguzi kisha atatoa taarifa ya kiofisi na kama hata yeye atakuwa amehusika kwa uzembe wa namna yoyote yupo tayari kuchukuliwa hatua na kama ikibainika wasaidizi wake ndiyo chanzo basi atamuomba Waziri mwenye dhamana kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi yao.
Kufuatia tukio hilo, baadhi ya wadau wa hospitali hiyo pamoja na wananchi wameiomba serikali kupitia Waziri wa Afya kuchukua hatua kali za kisheria wote waliohusika na uzembe wa kifo cha mtoto huyo pamoja na wale wanaokula rushwa kwa wagonjwa kwani pia, tukio hili limehusishwa na rushwa ambapo E-FM ina taarifa zaidi juu ya tuhuma hizo za rushwa kwa baadhi ya wahudumu wa hospitali hiyo.
Pia hata Mheshimwa Waziri Mkuu amehusiswa kwenye ishu hii na kuombwa kuamliwa kuundwa kamati ya uchunguzi kuhusu uzembe wa kifo cha mtoto huyu na wale wote watakaobainika wamehusika basi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu ikiwa ni pamoja kufukuzwa ili iwe fundisho wa wahudumu wengine watakaobaki.
Wakati huohuo, Elizabeth, licha ya kupoteza mtoto wake, amesema anamuomba hata Waziri wa Afya awaongezee mishahara manesi aliowataja awali (Elizabeth na Hyasinta) kwa utendaji na uwajibikaji wao mzuri wa kazi kwani hata walipokuwa wanaondoka waliwaaga wagonjwa kwa kuwafariji na kuwatia moyo hali iliyowafanya baadhi ya wagonjwa kusikitika kwa kuondoka kwao.
Hata msimamo wa familia kuhusu tukio hilo imesema kuwa kwa sasa bado wanamuhangaikia mama huyo kwani hali yake bado ni mbya kufuatia kupatwa na mshtuko kuhusiana na kifo cha mtoto wake ambapo licha ya kwamba alikuwa na matatizo ya pressure na hili ndo limemuongezea hali hiyo na mara baada ya kupata nafuu basi wako tayari kulifikisha mbali suala hilo ikibidi hata kwa Mh Rais Jakaya Mrisho Kikwete watafikisha kilio chao.
Hii ndiyo sehemu ya kwanza ya taarifa hii ya kusikitisha lakini bado tutaendelea kuwataarifu hatua kwa hatu kwani Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dokta Luoga ambae ameomba kupewa muda wa kulifanyia uchunguzi wa kina na kubaini usiku ule ni wahudumu gani walikuwepo pamoja na mkuu wao manesi kasha atatoa taarifa za hatua zinazostahiri kuchukuliwa dhidi yao.
Pia E-fm Radio 93.7 kupitia kitengo maalum cha habari za uchunguzi na ndiyo waliovumbua skendo hii ya kusikitisha inaendelea kufanya jitihada za kumtafuta Waziri wa Afya kwa ili kumfikishia taarifa za Skendo hii pamoja ushahidi mwingine, lakini shukrani za pekee zimuendee Mwandishi Mkuu wa Kitengo hicho cha Habari za Uchunguzi ndani ya kituo cha E-fm Radio Bw Livingstone Mkoi ambae amelifatilia suala hili usiku na mchana kuhakikisha ushahidi unakamlika hadi habari hii inaruka hewani. Source: E-fm Radio
No comments:
Post a Comment